HII sasa ni jeuri ya fedha. Azam FC ina
orodha ya makocha watano inayofanya nao mazungumzo, kati yao Kocha
Mfaransa wa klabu tajiri Afrika, TP Mazembe, Patrice Carteron ndiye
anayesakwa kwa nguvu zote.
Hadi sasa Azam inafanya mazungumzo ya karibu na Carteron ambaye pia anainoa timu ya Taifa ya Mali.
Wengine ni makocha waliowahi kuinoa
Zambia, Dario Bonetti na Herve Renard ambaye ndiye aliyeipa Zambia
ubingwa wa Afrika mwaka 2012 na kwa sasa anaionoa FC Sochaux ya
Ufaransa.
Wengine ni Diego Gazito aliyeifikisha
Mazembe fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2010 na mkurugenzi wa
ufundi wa sasa wa Mazembe, Lamine Ndiaye.
Makocha hao wote ni wa viwango vya juu na yeyote atakayetua nchini ataweka rekodi ya mshahara.
Habari za uhakika kutoka Azam ni kwamba
viongozi wa Azam sasa wapo katika hatua za mwisho za kukubaliana na
Carteron ili ainoe timu hiyo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na
Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Kocha huyo ndiye anayewafundisha Watanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu katika kikosi cha Mazembe.
Azam inajipa matumaini kumnasa Carteron
mwenye umri wa miaka 43 kutokana na mafanikio anayoyapata akiwa na
Mazembe msimu huu katika Kombe la Shirikisho Afrika na kuifikisha timu
hiyo katika fainali ya michuano hiyo.
Carteron aliyewahi kuichezea kwa mkopo
Sunderland ya England mwaka 2001 akitokea AS Saint-Etienne ya Ufaransa
ameifikisha Mazembe fainali Novemba 23 mwaka huu itacheza na CS Sfaxien
ya Tunisia jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
katika mchezo wa kwanza na kurudiana wiki mbili baadaye.
Azam inajipanga kuvunja mkataba wa kocha huyo ambaye alijiunga na Mazembe Mei 22 mwaka huu.
Mawasiliano ya Azam na Bonetti, Renard na Gazito kwa sasa yamesimama baada ya nguvu kubwa kuelekezwa kwa Carteron na Ndiaye.
Makocha wengine Dorian Marin wa Romania,
Zdravko Logarusic wa Croatia aliyewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya, Fabio
Lopez wa Italia na Patrick Liewig wameiomba Azam iwape kazi waonyeshe
mambo mzunguko ujao.