YANGA walicheka baada ya kumsainisha
kiungo, Hassan Dilunga wa Ruvu Shooting aliyekuwa akinyatiwa pia na timu
za Simba na Azam FC.
Mpaka sasa Yanga imewasajili wachezaji wawili katika dirisha dogo akiwamo kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja.
Lakini kama kawaida, Simba imesawazisha na kusajili wachezaji wawili wa haraka haraka.
Jana Jumapili, Simba ilianza usajili kwa
kishindo cha aina yake baada ya kuiliza Mtibwa Sugar na kumuacha kocha,
Mecky Maxime, akitokwa jasho na kufura hasira.
Simba ililipa tiketi ya ndege kutoka
Zanzibar ili kuileta Dar es Salaam ‘injini’ na kiungo wa Mtibwa, Awadh
Juma na kumsainisha mkataba wa miaka miwili.
Kama hiyo haitoshi mchezaji huyo amesaini sambamba na straika Badru Ally aliyekuwa akiichezea Canal Suez ya Cairo, Misri.
Wachezaji hao wote wako kwenye timu ya
Taifa ya Zanzibar iliyopiga kambi kwenye hoteli ya Bwawani mjini Unguja
ikijiandaa kwa Kombe la Chalenji.
Awali, Badru ambaye yuko Dar es Salaam
kwa miezi sita sasa, alikuwa akifanya mazoezi binafsi. Alifanya
mazungumzo ya kujiunga na Azam FC lakini wakashindwana kwa kile
kilichodaiwa kuwa mchezaji huyo alitaka dau kubwa.
Usajili wa Badru unamaanisha kwamba
Zahoro Pazi na Sino Agustino ambao walishindwa kupata namba kwenye
kikosi cha kwanza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, sasa wana hali
tete zaidi na watalazimika kukesha mazoezini ili kupata namba. Awadh
ambaye ni kiungo mshambuliaji aliyeacha majonzi Mtibwa, huenda akaingia
kirahisi kwenye kikosi cha kwanza kwa vile kocha Abdallah Kibadeni ana
shida ya mchezaji wa aina yake.
Badru alisema: “Nimesaini Simba kwa
mkataba wa miaka miwili, nikiwa straika, lengo langu ni kuipigia Simba
mabao hadi klabu ifurahi.
“Nimesajili Simba kwa sababu ni klabu
ambayo nina mapenzi nayo kwa muda mrefu, hilo nitaridhihirisha kwa
vitendo wenyewe wataona na hawatajutia kunisajili.”
Kuhusu Azam alisema: “Nilifanya mazungumzo nao, lakini tulishindwa kufikia makubaliano.”