DAR ES SALAAM.
KAMATI ya Bunge ya Huduma za
Jamii, imevikataa viwango vipya vya alama za ufaulu kwa elimu ya
sekondari vilivyotarajiwa kuanza kutumika mwaka huu na kutaka utaratibu
na alama zilizotumika mwaka jana, zitumike kupanga matokeo ya Mtihani wa
Taifa wa Kidato cha Nne wa mwaka huu.
Serikali ilitangaza utaratibu mpya wa alama za
Mitihani ya Kidato cha Nne na Sita kwa kufuta Daraja la Sifuri na kuleta
Daraja la Tano.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stephen
Ngonyani alisema jana kuwa kamati hiyo ilichukua uamuzi huo kwa kuwa
pamoja na udhaifu ulio kwenye alama hizo, kamati yao haikuhusishwa
katika mchakato wa kuandaa alama hizo.
“Mwenyekiti wangu (Margaret Sitta) alisema kile
hakiwezekani, kuna viwango ambavyo wameleta havipo kwenye nchi nyingine
duniani, tumewaambia wakavifanyie kazi walete tena,” alisema mbunge huyo
wa Korogwe Vijijini, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Profesa Maji
Marefu.
Ngonyani alisema waliagiza watendaji wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha wanaishirikisha kamati yao kwani
imejaa walimu wanaoweza kushauri vizuri.
“Hatutaki watuletee mambo ambayo yamewashinda baada ya kuyapeleka kwa wananchi,” alisema Ngonyani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Sifuni Mchome akitangaza uamuzi huo mapema mwezi huu,
alisema uamuzi wa kubadilisha mfumo huo umechukuliwa kutokana na
changamoto zilizojitokeza mwaka 2012.
Alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), katika kupanga matokeo hayo, kwa Kidato cha
Nne ni A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F 0-34 kwa upande wa Kidato
cha Sita, A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F=
0-39.
Alama mpya zilizotangazwa ni A=75-100, B+=60-74,
B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19. Alama hizo ni kwa kidato
cha nne na sita.
Kwa utaratibu huo, A ilitafsiriwa kuwa ni ufaulu
uliojipambanua, B+ ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu
mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.
Katika utaratibu huo, mtihani wa mwisho
ulitarajiwa kuwa na alama 60 na alama 40 zitokane na alama za Maendeleo
ya Mwanafunzi Shuleni (Continuous Assessment-CA).
Mwaka jana baada ya Serikali kufuta matokeo ya
mtihani wa Kidato cha Nne, Necta ilitumia CA ya 30 huku mtihani wa
mwisho ukiwa na alama 70. MWANANCHI