Dar es Salaam. Marekani imetoa ripoti
inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2013, huku ikiitaja
Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa wasichana, kuwatumikisha katika ngono
na usafirishaji wa binadamu.
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi
hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in
Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha
wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani
na biashara ya ngono.Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo
inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action),
pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake,
watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na
biashara ya ngono.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka
huu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka
bayana kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya
ndugu na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda
kuwasomesha au kuwatafutia ajira nzuri mijini.
“Unyonyaji wa wasichana wadogo na
utumikishaji majumbani ndilo tatizo linaloongoza, ingawa kesi za watoto
kusafirishwa kwa ajili ya biashara ya ngono katika mpaka wa Tanzania na
Kenya zinaongezeka. Pia, wasichana wananyonywa kwenye maeneo ya utalii,”
inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka
Burundi na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India
wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani
nchini Tanzania.
“Baadhi ya raia kutoka nchi jirani
huingia Tanzania kwa hiari yao, lakini hulazimishwa kufanya kazi
majumbani kabla ya kupelekwa kutumikishwa kwenye biashara ya ngono
Afrika Kusini, Ulaya na Mashariki ya Kati,” inaeleza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela
Kairuki alimtaka mwandishi kumtumia ripoti hiyo kwa njia ya baruapepe
ili aweze kuisoma na kuitolea maelezo.
Alipotafutwa siku ya pili, alisema kuwa
ameipokea na kuikabidhi ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) ili
ifanyiwe kazi na baadaye kutoa majibu.
“Ripoti niliipata nikaikabidhi ofisi ya
DPP kwa kuwa wao ndio wanaoweza kuitolea maelezo baada ya kuisoma. Maoni
yangu lazima yawe ya kitaalamu siwezi kusema bila kupata taarifa kutoka
kwao,” alisema.
Lawama kwa Serikali
Ripoti hiyo inaitupia lawama Tanzania
kwa kutokuwa na sheria thabiti za kupambana na biashara haramu ya
kusafirisha binadamu, huku ikitolea mfano namna ilivyoshindwa kuwasaidia
raia wake waliokuwa wakinyanyaswa nje ya nchi.
“Kamati ya Serikali ya kupambana na
usafirishaji binadamu, haijachukua hatua za kutosha katika kutekeleza
mpango mkakati wa kupambana na vitendo hivyo,” inaeleza na kuongeza:
“Serikali imeshindwa kutenga fedha kwa
ajili ya kuwasaidia waathirika wa usafirishaji wa binadamu kama ambavyo
inaelekezwa kwenye sheria ya kudhibiti biashara hiyo ya 2008.”
Taarifa hiyo inaitaka Tanzania kuongeza
nguvu katika kutekeleza sheria ya kudhibiti biashara ya kusafirisha
binadamu ya 2008 kwa kuwakamata na kuwashtaki wahusika wote, lakini
ikaikosoa kwa kusema inatoa adhabu ndogo kwa mtu anayebainika kufanya
makosa, ikiwa ni pamoja na kumhukumu kwenda jela miaka 10, kulipa faini
au vyote viwili kwa pamoja.
“Sheria hiyo haifanani na nyingine kama
za mtu anayepatikana na kosa la kubaka au kufanya kosa jingine la jinai.
Mamlaka imesema ina kesi nne inazozichunguza, saba zipo mahakamani toka
mwaka jana, zikiwepo mbili mpya,” inasema ripoti.
Pia, Serikali ya Tanzania imelaumiwa kwa
kushindwa kuripoti maendeleo ya uchunguzi wa maofisa wake waliotuhumiwa
kujihusisha na biashara ya usafirishaji binadamu.
LHRC na TGNP
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema tatizo la
usafirishaji wa binadamu pia linachangiwa na wasichana kuwa na tamaa ya
maisha mazuri, hivyo kukubali ahadi ambazo hupewa kwamba wanapelekwa
kusoma, wasifahamu wanarubuniwa.
“Wengi wanatamani kwenda ‘majuu’
wakidhani watapata elimu, lakini baadaye wanaingizwa kwenye vitendo
vinavyowafedhehesha na kuwafanya wakate tamaa kabisa,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema katika siku za karibuni
kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wasichana
waliochukuliwa vijijini kwenda mijini kufanya kazi.
Alisema pamoja na tatizo hilo kuongezeka
hapa nchini, hakuna tafiti za kutosha ambazo zimefanywa na wadau
mbalimbali kuonyesha madhara yaliyopatikana hadi sasa.
“Katika siku za usoni kumekuwa na
ongezeko kubwa la vitendo vya kunyimwa chakula, kupigwa na kufukuzwa
kazi huku wasichana wengine wakitumika kwenye biashara ya ngono,”
alisema na kuongeza:
“Ripoti hii isiishie kwenye makabrasha bali ifanyiwe kazi ili jamii yote ijue kuwa hili ni tatizo.”
Ripoti hiyo inabainisha kuwa watu 47,000
pekee ndio walioweza kuokolewa mwaka jana kutoka kwenye mazingira ya
utumikishwaji kati ya milioni 27 waliopo katika hali hiyo duniani.
Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa
nchi 44 ambazo zinajaribu kupambana na biashara hiyo, lakini hali
inazidi kuwa mbaya zaidi.
-Mwananchi