TABIA ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, kumrushia madongo Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya chama hicho, Zitto Kabwe, imesababisha hasira kwa mlengwa na sasa ameamua kuchukua uamuzi mkali zaidi.
Zitto
Kabwe pamoja na Mwanasheria wake,Albert Msando (kulia) wakiwasili
katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam jana wakiongozana na wafuasi
wanaopinga kuvuliwa uongozi wake, tayari kwa kwenda kusikiliza hukumu ya
kesi yake.
Zitto, ameamua kumrudi Lissu kwa staili nyingine kwa kwenda moja kwa
moja na kummaliza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa sababu anayo
makombora mengi makali ambayo hapo kabla aliyaficha ili kunusuru chama.Chanzo chetu kimesema, Zitto amekasirishwa na mashambulizi kutoka kwa Lissu na kwamba baada ya kukaa kimya muda mrefu, sasa uzalendo umemshinda, kwa hiyo kinachofuata ni mashambulizi mwanzo mwisho dhidi ya Mbowe.
“Huu ni mpango endelevu, Zitto anajua kwamba maneno ya Lissu ni ya kulishwa, mhusika ni Mbowe, ndiyo maana amesema hataki majibishano na kifaranga, anamtaka mama wa kifaranga ajitokeze,” alisema rafiki wa Zitto kwa sharti la kutotajwa jina na kuongeza:
“Mpango uliopo ni kukabiliana na mama wa vifaranga, yapo mabomu mengi ya maana ambayo Zitto anayo dhidi ya Mbowe, anachosubiri ni hukumu ya pingamizi lake mahakamani kuhusu Kamati Kuu ya Chadema kujadili uanachama mpaka itakampo fursa ya kukata rufaa Baraza Kuu.”
Hukumu hiyo, ilitarajiwa kusomwa jana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji John Utamwa.
Jumapili iliyopita, Zitto alisema kuwa maneno yanayozungumzwa na viongozi wa Chadema, mengi yakipitia kwenye kinywa cha Lissu ni sawa na mipasho kwa sababu hayamo kwenye tuhuma 11 ambazo walimwandikia azijibu kwa maandishi.
Kwa upande wa Mbowe, alinukuliwa akisema kuwa Zitto hapaswi kuibua tuhuma mpya dhidi yake, isipokuwa anachopaswa kufanya ni kujibu yale ambayo anatuhumiwa, huku akiyaita maneno ya mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini ni ya kitoto.