MUME AMKATA MKEWE PANGA MGUUNI KISA KUMZUIA MTOTO KUKEKETWA
MKAZI wa Kitongoji cha Songa Mbele wilayani Tarime mkoani Mara, Modester Mwita,33, amepigwa panga na mumewe kwa madai kuwa hataki mtoto wake wa kike wa umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) kwenda kukeketwa.
Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita akiwa Hospitali ya Bomani mjini hapa, Modester alisema kuwa tukio hilo lilitokea asubuhi saa mbili Desemba,13, mwaka jana baada ya kukataa mtoto wake huyo asikeketwe.
“Nilimwambia mume wangu Mwita Daudi kwamba haiwezekani mtoto wetu kwenda kukeketwa kwa kuwa mila hiyo imepitwa na wakati jambo ambalo lilimfanya kupatwa na hasira na kunikatakata kwa panga mguu,” alisema.
Modester aliongeza kuwa alikuwa ameenda mnadani Nyamwigura kupeleka biashara siku ya Desemba 12, aliporudi jioni nyumbani alikuta binti yake na mumewe hawapo ndipo mdogo wake akamwambia mwanaye alipelekwa kukeketwa.
‘’Mume wangu aliporudi nyumbani asubuhi nilimuuliza alikokuwa mwanangu hakunijibu, nilipomueleza kuwa sitaki akeketwe akaanza kunipiga na kunikimbiza kwa panga,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Aliponikamata alinikatakata mguuni, wasamaria wema wakanileta hapa Hospitali ya Bomani, yeye ametoroka na sijui hali ya binti yangu huko aliko ikoje,” alisema.
Afisa mmoja wa polisi ambaye hakupenda jila lake liandikwe kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi la polisi mkoani humo, amethibitisha kutokea kwa tukio na kuongeza kuwa mtuhumiwa anasakwa ili aweze kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazomkabili.