MWANGA ANASWA NA POLISI USIKU WA MANANE
Mtu mmoja asiyefahamika jina anayedaiwa kuwa ni mwanga amenaswa na polisi baada ya kudondoka katika eneo la Ilala Bungoni, jijini Dar akiwa kama alivyozaliwa.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita kuamkia Jumapili saa kumi usiku wakati mtu huyo alipodaiwa kudondoka akiwa na ungo, hirizi na kusabababisha watu waliokuwa eneo hilo kutahamaki.
Chanzo chetu kimesema kuwa, mara baada ya mtu huyo kudondoka watu waliitana na kukusanyika na wengine kutoa taarifa jeshi la polisi kwa njia ya simu ambao walifika haraka.
Watu waliokuwa katika eneo hilo walishangaa kuona mtu wa namna hiyo ametokea kusikojulikana na kuanguka na vitu ambavyo inadaiwa ni vya kiuchawi.
Askari polisi waliofika eneo la tukio walifanya kazi ya ziada kuzuia watu waliokuwa na lengo la kumpiga mtu huyo aliyeonekana kutojitambua kwa madai kuwa ni kwa sababu ya kudondoka kutoka angani.
Polisi walipomhoji hakuweza kutaja jina lake wala kuongea lolote hali ambayo iliwalazimu askari hao kumpeleka katika Kituo cha Polisi Pangani, Ilala kwa uchunguzi zaidi.
“Hili ni tukio la kwanza kutokea hapa na limetushangaza sana, tunaamini kuwa alidondoka kwa sababu tulisikia kishindo na tulipokuja kuangalia ni nini tukamkuta mtu huyu akiwa na hirizi, ungo na tunguri, alitueleza kwa tabu kuwa alikuwa na wenzake,” alisema shuhuda mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Juma Hussein.
Naye Asha Hamisi alisema mtu huyo wamaamini kuwa ni mwanga kwa kuwa alikuwa na vitu vinavyofanywa na wachawi au waganga.
“Hapa alipoangukia ndipo ninapofanyia biashara na tangu adondoke nakosa wateja kabisa tofauti na zamani, hali hii naamini imetokana na kudondoka kwa mtu huyo,…serikali sasa ijue kuwa uchawi upo,” alisema Asha.