MWILI wa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi umewasili hivi punde jijini Dar es Salaam kutoka nchini Afrika Kusini alipofia akiuguza majeraha.
Dkt. Mvungi alifariki (Jumanne, Novemba 12, 2013) katika Hospitali ya Millpark jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.
Kesho, Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika Ibada ya mazishi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana.
Aidha, Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku ya Jumapili, Novemba 17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu, Novemba 18, 2013.