Muigizaji maarufu wa filamu Tanzania (Bongo Movie) Steve
Nyerere amesema maisha ya kifahari wanayoonesha wasanii wengi wa kike wa
filamu sio maisha halisi yanayotokana na kazi ya filamu wanayofanya.
Akiongea kwenye kipindi cha Sun Rise cha 100.5 Times fm, Steve
amesema watu wasiangalie maisha ya kifahari yanayooneshwa na baadhi ya
wasanii kwenye magazeti wakadhani kuwa yanatokana na kipato cha filamu
wanazofanya.
“Sisi wanaume upande wa Bongo Movie kupata hela tunategemea movies
zetu, dada zetu wanahongwa pesa ambapo sisi wanaume
hatuwezi kuhongwa.” Alisema Steve Nyerere.
“Watakuja tu watu wametoka Mererani, wametoka Buzwagi, watakuja watu
wametoka wapi kule…wanamtaka dada fulani, kwanza hawawezi kuja pale
wakasema 10 hii hapa…dada zetu ni watu wa show shine unawajua tena
lazima waoshe. Anunue cheni atoe kwenye gazeti, anunue nini..sasa
wanavyoona kwenye magazeti wanadhani hawa watu ndivyo wanavyoishi,
wakati sio hivyo," amefunguka.
Msanii huyo ambaye ni moja kati ya wachekeshaji wakubwa nchini
aliwalinganisha wasanii wa kike na wasanii wa kiume kwa kuwataja majina
kama mfano.
“Leo huwezi kumfananisha JB na Wolper au na Wema, huwezi kumfanisha
Steve Nyerere na Shilole, huwezi kuwafananisha hao watu. Kwa sababu yeye
ana njia nyingi, kwa sababu yeye kwa siku anaweza akapigiwa simu 34,
mimi kwa siku nikapigiwa simu moja tu na producer.”
Muigizaji huyo ambaye pia ni kiongozi katika Bongo Movie Club
amewaomba viongozi wa serikali kutoangalia pesa vitu vya kifahari
ambavyo zinaandikwa kwenye magazeti na au vinavyonunuliwa na wasanii wa
filamu na kuwaza kuwa kuna pesa nyingi imekumbatiwa kwenye tasnia hiyo,
na kwamba hali halisi haiko hivyo.
Ameongeza kuwa wasanii bado wanaibiwa sana kazi zao na wanaofaidika
zaidi ni watu wanaoiba kazi zao, hivyo serikali iwaangalie kabla ya
kuwaza kupata pesa kutoka kwao.
Steve amesema anajipanga kufanya filamu ya 'Good Bye Mr. President', inayohusu Rais Jakaya kuwaaga watanzania.