ZANZIBAR
NOVEMBA 15, 2013. Jeshi la Polisi Zanzibar limewakamata watuhumiwa
wemgine watatu wakiwemo Maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA
kituo cha Bandari Zanzibar kwa kuhusika na kashfa ya kupatikana kwa meno
ya tembo yenye thamani ya Mabilioni ya shilingi.
Kamishna
wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, amewataja Maafisa hao wa TRA
waliokamatwa kuwa ni Omari Hamad Ali(50) na Mohammed Hija(48) ambao wote
wanafanyia kazi katika Bandari ya Zanzibar. Mtuhumiwa mwingine ni
kibarua wa Mamlaka ya bandari Zanzibar Haidar Ahmad Abdallah(54).
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunaifanya idadi ya watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa kwa kuhusika na sakata hilo kufikia watano.
Kamishna
Mussa amesema Watuhumiwa wengine wawili ambao ni wafanyakazi wa Kampuni
ya Uwakala wa Mizigo ya Island Sea Food Limited, Mohammed Suleiman
Mussa(45) na Juma Ali Makame(34) wao walikamatwa siku ya tukio la
kukamatwa kwa meno hayo ya tembo kwenye Bandari ya Zanzibar.
Tayari watuhumiwa hao wamesafirishwa kwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi.Pamoja
na mambo mengine, kusafirishwa kwa watuhumiwa hao kwenda Jijini Dar es
Salaam, kunatokana na Zanzibar kutokuwa na Sheria maalumu inayohusu
wanyamapori.
Maafisa wa Idara ya Wanyamapori nchini, leo wamekamilisha kazi ya kuhesabu
na kulinganisha vipande 1,023 vya meno ya tembo vilivyokamatwa jana
kwenye Bandari ya Zanzibar na kubaini idadi ya tembo waliouawa kuwa ni
305.
Meno
hao yenye uzito wa kilo 2,915 yenye thamani ya Dolla 4,775,000 sawa na
shilingi 7,480,125,000 za Tanzania (Bil.7.4), yalikamatwa juzi yakiwa
yamehifadhiwa katika magunia 98 na kuwekwa kwenye konteina moja la futi
40 lenye namba PCIU 857619/0 lillilokuwa tayari kupakiwa kwenye meli ya
MV Kota Henning kupelekwa nchini Ufilipino kwa magendo.
Hadi
sasa bado Makachero wa Polisi wa Kimataifa Interpol hapa nchini kwa
kushirikiana na Makachero wa Polisi Zanzibar, idara ya wanyamapori makao
makuu wanaendelea na upelelezi wa kuwabaini wale wote waliohusika na
kashfa hiyo.
Jana
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa kazi kubwa
iliyobaki ni kuhakikisha kuwa upelelezi wa kina unafanyika ili
kuwakamata wale wote wanaohusika na mtandao huo.
Alisema
hadi sasa Jeshi la Polisi bado linamsaka tajiri aliyewezesha mipango ya
kukusanywa na kusafirisha shehena hiyo kutoka Tanzania Bara hadi
Zanzibar ili kusafirishwa nje ya nchi.