WAKATI taifa likiwa katika msiba kufuatia kifo cha Waziri wa Fedha,
Mipango na Uchumi, Dk. William Mgimwa, wananchi wameitaka serikali
kueleza kwa nini kwa kipindi chote cha kuumwa kwake, ugonjwa uliomuua
ulifanywa siri.
Waziri Mgimwa alifariki dunia Jumatano (juzi) saa 5:20 asubuhi kwa
saa za Afrika Kusini (Tanzania saa 6:20) katika Hospitali ya Mediclinic
Klooff jijini Johannesburg nchini humo.
Vyanzo mbalimbali kutoka wizara hiyo vinasema, waziri Mgimwa ambaye
pia ni mbunge wa Jimbo la Kalenga, Iringa, kabla ya kuugua alikuwa na
wakati mgumu kiutendaji kutokana na shinikizo mbalimbali alizokuwa
akizipata.
“Kuna mambo sana pale wizarani, waziri alikuwa na wakati mgumu sana,
haya mambo ndiyo yalimfanya hata akajikuta anapata matatizo na kuugua,”
kilisema chanzo hicho ambacho kilikataa kutoa ufafanuzi zaidi wa mambo
hayo yaliyomtokea kiongozi huyo.
Ijumaa liliwasiliana na daktari mmoja bingwa wa magonjwa ya binadamu
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuulizwa kama mtu ambaye
ana matatizo ya mara kwa mara kazini kwake na kufokewa au kupewa amri
anaweza kupata na tatizo gani, akafafanua.
Akifafanua zaidi, daktari huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake
gazetini alisema upo uwezekano wa marehemu Mgimwa kuwa alipata ugonjwa
unaosababishwa na damu kuganda na kuziba kwenye njia ya mishipa.
“Kama mnasema alikuwa akipata shinikizo huko kazini kwake, basi
huenda alitokewa na kitu kinachoitwa kitaalam Trans Ischaemic Attack
(TIA). Hii ni hali ya damu au mafuta kuganda na kuziba kwenye mishipa,
hivyo kusababisha damu kushindwa kutembea kuelekea sehemu mbalimbali
kwenye mfumo wa ubongo,” alisema daktari huyo na kuongeza:
“Mara nyingi watu wanaopata tatizo hilo husababishwa na kupewa
taarifa za kushtua kama kufokewa au kugombeshwa na kusababisha msongo wa
mawazo.”
Akitoa ufafanuzi zaidi, daktari huyo alisema, TIA huweza kumtokea mtu
yeyote na kwamba kwa kawaida, hudumu kati ya dakika moja hadi tano na
anayekutwa na hali hiyo, kama asipopatiwa tiba mapema, huwa katika
hatari ya kupata ugonjwa wa kupooza (stroke).
“Lakini kama hali hiyo itaendelea kuwepo pasipo damu au mafuta
yaliyoganda kuyeyuka, basi mishipa hushindwa kupitisha damu kuelekea
sehemu za ubongo na hivyo kusababisha eneo hilo kufa. Kadiri TIA
inavyokaa muda mrefu ndivyo madhara yanavyokuwa makubwa ya kuweza
kusababisha kupooza au hata kifo,” alisema.
Hata hivyo, wananchi wameishauri serikali kuweka wazi taarifa za
maradhi ya viongozi wa ngazi za kitaifa ili kuondoa sintofahamu mitaani.